Kocha mpya wa Yanga Mzambia George Lwandamina amefunguka kuhusu kikosi cha timu hiyo na kusema kwa kiasi fulani amefurahishwa na wachezaji waliopo japo kuna mapungufu kadhaa ya kuyafanyia kazi kutokana na video kadhaa alizoangalia.
Mzambia huyo ambaye anasifika kwa soka la kasi na pasi nyingi anatarajia kuanza kazi punde tu baada ya wachezaji kurudi kutoka mapumzikoni tayari kwa raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano mingine.
"Nimekiona kikosi cha Yanga kupitia video za michezo yao iliyopita, ni timu nzuri japo ina mapungufu, nitapata muda mzuri zaidi pale nitapokutana na wachezaji na kuanza maandalizi," amesema Lwandamina.
Ameongeza kuwa punde tu atakapoanza kazi ataangalia sehemu gani ya kuongeza na kufanyia marekebisho ili kuleta tija zaidi kikosi na kuwa na timu yenye ushindani ndani na nje ya nchi.
"Yawezekana nikawatumia wachezaji hawa hawa ama nikasajili kutegemea mapungufu ntakayoyaona pindi ntakapo onana nao pia ripoti ya kocha aliyepita itanisaidia, wachezaji wanapaswa kutumia vema mapumziko haya kujifua zaidi pasipo kubweteka."
No comments:
Post a Comment